MATOKEO MAALUM YANAYOTARAJIWA
Kufikia mwisho wa mada, mwanafunzi aweze:-
- kutambua sauti za herufi mbili zilizofunzwa ili kuimarisha stadi ya kusikiliza na kuzungumza,
- kutamka sauti lengwa za herufi mbili katika kuimarisha stadi ya kuzungumza,
- kusoma herufi za sauti mbili ili kuimarisha usomaji bora,
- kusoma maneno kwa kutumia silabi zinazotokana na sauti lengwa ili kuimarisha usomaji bora,
- kusoma hadithi fupi zilizo na maneno yaliyo na sauti lengwa ili kuimarisha usomaji bora,
- kuandika maneno kutokana na herufi alizofunzwa ili kuimarisha stadi ya kuandika,
- kufurahia kutumia sauti zilizofunzwa katika mawasiliano.
MAPENDEKEZO YA SHUGHULI ZA UJIFUNZAJI
- Mwanafunzi atambue sauti /ch/ na /dh/ katika maneno.
- Mwanafunzi asikilize sauti lengwa zikitamkwa na mwalimu kisha atamke pamoja na mwalimu na mwishowe atamke akiwa peke yake, wawili wawili na kama darasa.
- Mwanafunzi aweza kutumia teknolojia kama vile papaya na DVD kusikiliza sauti zikitamkwa.
- Mwanafunzi atambue herufi zinazowakilisha sauti lengwa kwa kutumia kadi za herufi.
- Mwanafunzi aambatanishe silabi kusoma maneno yanayotokana na sauti lengwa.
- Mwanafunzi atenganishe silabi katika kutambua sehemu mbalimbali za maneno.
- Mwanafunzi aweza kumsikiliza mgeni mwalikwa akitamka sauti lengwa.
- Mwanafunzi aandike herufi za sauti alizosoma hewani na vitabuni.
- Mwanafunzi asome maneno kwa kutumia silabi na kuchanganua yaliyo marefu zaidi.
- Wanafunzi wasome hadithi zilizo na maneno yaliyobeba sauti lengwa wakiwa wawili wawili.
- Mwanafunzi aweza kutumia vifaa vya kiteknolojia kama vile tarakilishi, projekta kipasasauti na rununu kusikiliza na kusoma hadithi.
- Mwanafunzi aweza kufinyanga maumbo ya herufi inayowakilisha sauti lengwa.
- Mwanafunzi anakili herufi na maneno yanayotokana na sauti alizofunzwa.
MASWALI DADISI
- Ni sauti zipi unazojua kutamka?
- Unajua kusoma silabi na maneno yapi?
- Unajua kuandika silabi na maneno yapi?
Umilisi wa kimsingi unaokuzwa:
mawasiliano na ushirikiano – wanafunzi wanashiriki katika kazi za vikundi ujuzi wa kidijitali – matumizi ya teknolojia katika kujifunza hamu ya kujifunza: mwanafunzi atapata hamu ya kutaka kutumia vipengee vilivyofunzwa vya sarufi kwenye mawasiliano ubunifu – mwanafunzi anatumia ubunifu katika kutunga sentensi na masimulizi.
Uhusiano na masuala Mtambuko:
elimu ya maendeleo endelevu- usalama katika usafiri –wanashughulikia vyombo vya usafiri.
Uhusiano na Masomo Mengine:
Environmental Activities na English Activities
Mapendekezo ya shughuli zingine zilizoratibiwa za ujifunzaji:
- kazi ya vikundi
- michezo
- mashairi na nyimbo kuhusu usafiri
Uhusiano na Maadili:
uwajibikaji heshima.
Mapendekezo ya shughuli za huduma za kijamii zinazochangia ujifunzaji: kuwahamasisha wengine kuhusu usalama barabarani.
Mapendekezo ya Tathmini:
- kuchunguza anavyotamka sauti zilizofunzwa
- kuuliza maswali kuhusu vyombo vya usafiri
- kuchunguza jinsi mwanafunzi anavyojibu maswali ya masimulizi na hadithi na kutoa muhtasari wa hadithi aliyosomewa au kusimuliwa
- kuchunguza jinsi anavyotumia herufi kubwa kuakifisha maneno na sentensi.
Viwango vya Kuzingatia katika Kutathmini
Kuzidisha Matarajio
Mwanafunzi,
- anatamka sauti lengwa kwa ufasaha
- anataja majina ya vyombo vya usafiri kwa wepesi
- anatumia msamiati wa usafiri kwa ubunifu katika sentensi
- anasoma kwa ufasaha.
- anafahamu kwa urahisi hadithi aliyosimuliwa, aliyosoma na kusomewa
- anatumia herufi kubwa ipasavyo katika kuakifisha maneno na sentensi kwa wakati
- anaandika kwa hati nadhifu na kwa haraka.
Kufikia Matarajio
Mwanafunzi,
- anatamka sauti lengwa vyema
- anataja majina ya vyombo vya
usafiri
- anatumia msamiati wa usafiri ifaavyo katika sentensi
- anasoma ifaavyo
- anafahamu hadithi aliyosimuliwa, aliyosoma na kusomewa
- anatumia herufi kubwa ipasavyo katika kuakifisha maneno na sentensi
- anaandika kwa hati bora.
Kukaribia Matarajio
Mwanafunzi,
- ana changamoto katika kutamka baadhi ya sauti lengwa vyema
- anataja baadhi ya majina ya vyombo vya usafiri
- ana changamoto katika kutumia baadhi ya msamiati wa usafiri kwenye sentensi
- anasoma baadhi ya kazi anazopewa
- anafahamu baadhi ya hadithi alizosimuliwa, aliyosoma au kusomewa
- ana changamoto kiasi katika kuakifisha maneno na sentensi kwa kutumia herufi kubwa
- anaandika kwa hati zinazosomeka.
Mbali na Matarajio
Mwanafunzi,
- ana changamoto katika kutamka sauti lengwa
- ana changamoto katika kutaja baadhi ya majina ya vyombo vya usafiri
- ana changamoto katika kutumia msamiati wa usafiri kwenye sentensi
- ana changamoto katika kusoma
- ana changamoto katika kufahamu hadithi aliyosimuliwa, aliyosoma au kusomewa
- ana changamoto katika kuakifisha maneno na sentensi kwa kutumia herufi kubwa
- ana changamoto katika kuandika.